Back to top

Mtoto wa mganga afa kwa kunywa dawa ya mvuto wa mapenzi.

18 January 2021
Share

Juma Dela umri miaka 12 amefariki dunia na wengine 2 kunusurika kifo wilayani Kahama baada ya kunywa dawa ya kienyeji waliopewa na mganga kwa ajili ya kuogea, lengo likiwa kusafisha nyota ya Kimapenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba amethibitisha kutokea tukio hilo ambapo amesema jeshi hilo linamsaka mganga huyo Bwana Dela Megejuwa Lwaho miaka 44 ambaye ni baba mzazi wa mtoto Juma Dela (12) aliyefariki kwa kunywa dawa hiyo ya kusafisha nyota ya Kimapenzi, ambaye amekimbia.

Amesema jeshi hilo linamsaka mganga huyo ili pia kumchunguza kama ana vibali vya kufanya kazi hiyo, huku likisema kuwa watu wawili walionusurika kifo walikuwa ni wateja tu ambao walifika kwa mzee huyo kupatiwa huduma.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya halmashauri ya Mji wa Kahama kwa uchunguzi, huku watu hao wawili walionusurika kifo wakipatiwa matibabu katika kituo cha afya Chela.