Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amewahimiza wananchi wa Mufindi mkoani Iringa kuhakikisha wanafuga ng’ombe wa maziwa kwa ajili ya kujipatia kipato.
Ulega alisema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta inayoshughulikia migogoro ya Matumizi ya Ardhi katika vijiji 975 ilipofanya ziara katika kijiji cha Kibengu wilayani Mufindi mkoa wa Iringa.
Naibu Waziri Ulega amesema ni vyema wananchi wa Mufindi na wilaya nyingine za mkoa huo wanapomaliza kutumia mahindi basi wawe na maziwa ambayo sehemu yanaweza kutumiwa na watoto na kiasi kingine kikatumika kwa ajili ya biashara.
Alisema, mbali na juhudi mbalimbali zinazofanywa katika kuboresha sekta ya mifugo lakini moja ya jambo wizara yake itafanya ni kuzungumza na uongozi wa mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na kiwanda cha maziwa cha Asasi na Benki ya Kilimo pamoja na Shirika la PASS ni kuanzisha mradi ambao wale wananchi walio tayari basi waweze kukopeshwa ng’ombe wa maziwa.