
Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wazee wa Jimbo la Bumbuli, Mkoani Tanga, wameibuka na ahadi ya kumchukulia fomu ya kugombea ubunge kwa Mbunge wao wa sasa, January Makamba kwa kutumia fedha zao binafsi kama ishara ya kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya jimbo hilo kwa ushirikiano na Rais Samia Suluhu Hassan.
Azimio hilo wamelitoa katika mkutano maalum wa pamoja wenye lengo la kujadili maendeleo ya Bumbuli, wazee na viongozi hao wamesema wametoa azimio hilo baada ya kufanya tathmini kwa wakazi jimbo hilo nakuona kuwa matakwa ya wananchi bado wanataka Mbunge aliyopo sasa aendelee kuongoza kipindi kijacho cha 2025 - 2030 ili aendelee kumsaidia kazi Rais Samia.
“Mchango wa January katika maendeleo ya Bumbuli ni wa kipekee. Huyu si kiongozi wa maneno, bali wa vitendo. Muda ukifika, sisi wenyewe tutamchukulia fomu ya ubunge.” alisema mmoja wa wazee kwa msisitizo.
Awali , Katibu wa Wenyeviti wa CCM wa kata za Bumbuli, Baraka Utanda, akisoma azimio rasmi la pamoja la kuunga mkono Makamba kuendelea kuwa Mbunge wa Bumbuli kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
“Tumeazimia kwa kauli moja kwamba kwa kipindi cha 2025 hadi 2030, tutampigia kura Rais Samia tutampigia kura tena January Makamba. Tumemwona anavyojali maendeleo, na hatutaki kupoteza kiongozi wa aina hii,” alisema Utanda.
January Makamba, amekuwa mbunge wa Bumbuli kwa vipindi kadhaa na amepongezwa mara kadhaa kwa kusukuma miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, miundombinu na nishati lakini ndie aliyepambana bumbuli kuwa halmashauri kamili.