Back to top

PINDA ATAKA MRADI UJENZI CHUO CHA ARDHI MOROGORO KUWEKEWA NGUVU

29 June 2024
Share

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Geophrey Pinda, ametaka mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ardhi Morogoro unaojumuisha eneo mahali chuo kilipo na eneo la mlima Kola, kuwekewa nguvu ili uweze kukamilika kabla ya muda uliopangwa.

Mhe.Pinda ametoa kauli hiyo leo wakati alipokwenda kukagua eneo la ujenzi wa mradi huo katika eneo la mlima Kola mkoani Morogoro.

Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ardhi Morogoro, unaojumisha mahali chuo kilipo pamoja na eneo la Mlima Kola umeelezwa kuchukua miaka 20 mpaka kukamilika kwake mwaka 2043 na utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 70 ambapo bilioni 64 zitawekezwa eneo la mlima Kola na bil 6 kwenye kampasi ya chuo Kilakala.

Mradi huo unajumuisha Jengo la Utawala, Madarasa, Maktaba, Hosteli za Wanafunzi, Kumbi kubwa za kufundishia, Zahanati, Migahawa pamoja na maeneo ya kuabudia.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Idara ya Taaluma Pius Kafefa, vyanzo vya mapato kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo wa chuo cha ARIMO  ni ada za wanafunzi, miradi mbalimbali ya chuo kama vile ushauri wa kitaaluma, fedha kutoka serikalini pamoja na maombi  kutoka kwa wafadhili.

Naibu Waziri wa Ardhi Mhe. Pinda amesema, ni vyema mradi huo ukawekewa nguvu ili uende kwa haraka kwa kuwa kuchukua muda mrefu kutafifisha uharaka wa maendeleo ya chuo.