Back to top

WAZIRI JENISTA AKAGUA HOSPITALI KUELEKEA MKUTANO WA NISHATI

26 January 2025
Share

Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, leo amefanya ziara hospitali Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), na Hospitali ya Agakhan ili kukagua na kuridhishwa utayari wa kutoa huduma kwa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mkutano wa Nishati utakaofanyika Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 27 hadi 28 Januari, 2025.

Katika ziara hiyo, Mhe. Mhagama ameeleza kuridhishwa kwake na juhudi za hospitali hizo ambazo ziko tayari kutoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi endapo itatokea Kiongozi yoyote au Mkuu wa Nchi yeyote atakayehitaji kuhudumiwa kulingana na dharura yoyote endapo itajitokeza.

“Mkutano huo utawakutanisha viongozi wakuu wa nchi mbalimbali, wataalam wa sekta ya nishati na wadau wa kimataifa hivyo ni muhimu kuhakikisha wageni wote wanapata huduma bora za afya iwapo itahitajika, katika hilo, Serikali tumejipanga vizuri” amesisitiza Mhe. Mhagama.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi amesema hospitali hiyo imejipanga vizuri kupitia Idara ya Tiba na Magonjwa ya Dharura ambayo ndiyo yenye watalaam wabobezi katika eneo hilo na kubwa kulizo zote nchini kuhakikisha inatoa huduma kwani ndiyo itakuwa inapokea wageni hao, kuwaimarisha na kisha kuwasambaza katika hospitali nyingine kulingana na shida aliyo nayo mgonjwa endapo itahitajika kufanya hivyo.

Mkutano huu ambao kauli mbiu yake ni Kuharikisha Upatikanaji wa Nishati  Afrika, umeandaliwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia, Benki ya Afrika ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Marais wa Nchi za Afrika 24, wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika 21, Wakuu wa Taasisi za Kimataifa 6, Washirika wa Maendeleo 5 watashiriki mkutano huo ambapo pia washiriki wengine 2,600 ndani na nje ya Tanzania wamejisajili kushiriki mkutano huo