Back to top

POLISI YABAINI MIPANGO YA CHADEMA KUVAMIA VITUO VYA POLISI

30 August 2024
Share

Wakati Sakata la Deusdedith Soka na wenzake wawili kutokujulikana walipo, huku Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi, Jeshi hilo limesema limepata taarifa za uhakika kuhusu viongozi wa CHADEMA kupanga vitendo vya kihalifu vinavyo hatarisha amani ya nchi, kwa kuhamasisha na kuunda vikundi vya vijana wapatao 20 ili wavamie vituo vya polisi vilivyopo Jijini Dar es Salaam kwa wakati mmoja.

Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini DCP, David Misime, imesema kuwa viongozi wa CHADEMA wamefanya kikao kwa njia ya Kielekroniki (zoom) na kukubaliana waanze kuhamasisha wafuasi wa chama hicho kufanya maandamano ya kuelekea maeneo mbalimbali zikiwemo ofisi.

DCP Misime amesema Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilieleza kuwa hakuna uthibitisho unaoonesha kuwa viongozi wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) wanashikiliwa na polisi na kuamuru viongozi hao kutafutwa mahali walipo, ndipo sasa wamebaini viongozi hao wa CHADEMA kuratibu maandamano kwa njia ya Zoom.

DCP Misime ametoa onyo kali kwa yeyote atakaye endelea kuratibu, kuhamasisha na kushiriki katika uhalifu huo wakupangwa, ambao lengo lake ni kutaka kuvuruga amani ya nchi, baada ya kushindwa kwa mikakati yao, hivyo atakayefika kituo chochote kwa nia ovu atashulikiwa ipashavyo kwa mujibu wa sheria.