Back to top

PURA YATAKIWA KUENDELEA KUNADI VITALU MAFUTA NA GESI

18 February 2025
Share

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli( PURA) kuendelea kuvutia  uwekezaji katika vitalu vilivyo wazi vya mafuta na gesi asilia ili kuongeza kiasi cha nishati hiyo nchini.

Mhe. Kapenga amesema hayo leo wilayani Morogoro, Mkoa wa Morogoro wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa PURA kinacholenga kujadili  masuala mbalimbali ikiwemoMpango na Bajeti ya Taasisi hiyo kwa mwaka  wa fedha 2025/26.

" Mkifanikiwa  kuvutia uwekezaji katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi, nchi itaongeza ugunduzi wa rasilimali hiyo muhimu ikiwa ni pamoja na kuogeza futi za ujazo wa gesi  inayopatikana nchini. Pia mkiendelea kuvutia uwekezaji kupitia Duru ya Tano ya kunadi vitalu itakayozinduliwa mwezi machi mwaka huu, pamoja na faida zilizopo, mtakuwa mmeendeleza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuifungua Tanzania kiuchumi na kuvutia uwekezaji zaidi."Amesema Kapinga

Amesema Wizara ya Nishati inatambua umuhimu wa tukio la Duru ya Tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini pamoja na kutambua kazi kubwa ambayo imeshafanyika kuelekea uzinduzi wa tukio hilo ambalo amesema kuwa ni muhimu katika 
 kuvutia uwekezaji zaidi katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini. 

“ Kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukizungumzia ugunduzi wa futi za ujazo trilioni 57.54 pekee ni wakati sasa wa kufanya zaidi na zaidi ili tuweze kuongeza ugunduzi wa rasilimali hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa." Amesisitiza Mhe.Kapinga

Katika kikao hicho cha  Baraza la Wafanyakazi,  ameupongeza uongozi wa PURA kwa kuendelea kuwashirikisha watumishi wake katika kujadili, kupanga na kupitisha mipango na Bajeti ya Taasisi kwenye Baraza la Wafanyakazi ikiwa ni utekelezaji pia wa Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma.

Amesema kufanyika kwa vikao hivyo ni ishara tosha ya utawala bora mahala pa kazi kwa kuwa watumishi wanapata fursa ya kuchangia mawazo yao kuhusu hali ya uendeshaji wa Taasisi hivyo kuendelea kuwa ni sehemu muhimu ya Taasisi. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli( PURA) Mhandisi. Charles Sangweni, amesema duru ya tano (5) ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na
gesi asilia nchini inatarajiwa kuzinduliwa mwezi Machi, 2025 Jijini Dar
es Salaam wakati wa Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Nchi
Wanachama wa Afrika Mashariki (EAPCE’25).

Amesema PURA inaendelea kusimamia na kudhibiti shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa gesi asilia katika vitalu mbalimbali nchini na Kuhakikisha watanzania wazawa wanashirikishwa katika miradi mbalimbali ya mkondo wa juu wa petroli nchini.