Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bw. David Beasley amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi mzuri, na kwamba WFP imedhamiria kutumia fursa hiyo kufanikisha utekelezaji wa mipango yake mbalimbali.
Bw. Beasley ambaye amewahi kuwa Gavana wa Jimbo la Carolina Kusini nchini Marekani amesema hayo leo tarehe 26 Julai, 2018 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli, kando ya ziara yake ya siku 7 hapa nchini.
“Tumezungumza kuhusu namna Tanzania inavyong’ara kimataifa, kuhusu WFP inavyoweza kushirikiana na Tanzania kuboresha maisha ya wakulima wadogo, kupata masoko na bei nzuri ya mazao ya wakulima wadogo na tunaamini Tanzania inaweza kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula kwa ajili ya ukanda wote wa Afrika, hivyo tunataka kutumia fursa ya ukarimu, ushirikiano na uongozi bora wa Mhe. Rais Magufuli na baraza lake la Mawaziri ambalo tunaamini wamedhamiria kuboresha maisha, kuongeza tija na kuondoa rushwa” amesema Bw. Beasley.
Bw. Beasley amebainisha kuwa pamoja na kununua mazao ya chakula kutoka kwa wakulima kila msimu, WFP inaendesha miradi ya kuwawezesha wakulima wadogo kuzalisha mazao bora na kwa tija nchini Tanzania na hivi sasa inao mpango wa kupanua uwigo kwa kuongeza idadi ya wakulima wanaofikiwa na mradi huo kutoka 50,000 hadi 250,000 katika miaka miwili ijayo.
Aidha, Bw. Beasley ameahidi kulifanyia kazi ombi la Mhe. Rais Magufuli la kutaka WFP iongeze kiwango cha mazao inayoyanunua kutoka kwa wakulima kutoka tani 56,000 za msimu uliopita, ikiwa ni juhudi za kukabiliana na changamoto ya wakulima kukosa soko la mazao ya chakula cha ziada kinachozalishwa hapa nchini.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amempongeza Bw. Beasley kwa kutembelea Tanzania na dhamira yake njema ya kushirikiana na Tanzania katika kuwasaidia wakulima wadogo wa mazao ya chakula, kuongeza kiwango cha mahindi yanayonunuliwa na WFP na pia kutumia bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mazao na mizigo mbalimbali ya nchi za ukanda huu.
Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na WFP hasa katika kukabiliana na changamoto ya wakulima kukosa soko la mazao ya ziada na amebainisha kuwa katika msimu huu Tanzania ina takribani tani milioni 4 za chakula cha ziada kinachopaswa kuuzwa nje ya nchi.
“Namshukuru sana kwa kuunga mkono juhudi tunazozifanya kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania, na hii ndio njia pekee ya kuhakikisha nchi inajikomboa kwa kuwa na uchumi wa kweli, kwani tumedhamiria kujitegemea, na pia namshukuru kwa kuunga mkono ‘Hapa Kazi Tu’ na juhudi zingine zote ikiwemo kupambana na rushwa na kwamba anaiona Tanzania ya pekee na yenye mwelekeo tofauti wa kuleta neema” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Bw. Beasley kuwa uchumi wa Tanzania unakuwa vizuri kwa wastani wa asilimia 7 na unatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 7.1 katika kipindi kifupi kijacho, mfumuko wa bei umeendelea kuwa kwa tarakimu moja (ukiwa umeshuka hadi kufikia asilimia 3.8), pia amemkaribisha kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii na kuwa balozi wa kuutangaza uzuri wa Tanzania.
Mazungumzo ya Mhe. Rais Magufuli na Bw. Beasley yamehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omar Mgumba na Mwakilishi Mkazi wa WFP hapa nchini Bw. Michael Dunford.