Back to top

Rais Samia aagiza uchunguzi chanzo cha moto soko la Kariakoo.

11 July 2021
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla na Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo kufuatia hasara kubwa waliyoipata kutokana na kuungua moto kwa Soko Kuu la Kariakoo lililopo Jijini Dar es Salaam.

Kufuatia hasara kubwa iliyotokana na kuungua kwa Soko hilo usiku wa Julai 10, 2021, Mhe. Rais Samia ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanya uchunguzi wa kina kujua chanzo cha moto huo. 

Amesema Soko kuu la Kariakoo ni soko kubwa Jijini Dar es salaam ambalo lina mkusanyiko mkubwa wa wafanyabiashara na kuteketea kwa soko hilo kutakuwa kumesababisha hasara kubwa kwa wapangaji na wamiliki wa soko hilo kongwe nchini.

Mhe. Rais Samia amesema Soko la Kariakoo licha ya kuajiri wafanyabiashara wengi lakini ni kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki hivyo tukio hilo si hasara kwa Wafanyabiashara tu bali hata kwa Serikali.

Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia ametoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martin Shigella na Jumuiya za Kiislaam Tanzania  kufuatia kuungua moto kwa Bweni la Shule ya Sekondari ya Kiislam ya Wasichana  AT  TOWN inayomilikiwa na Taasisi ya Kiislam iliyopo  mji Mpya katika Manispaa ya Morogoro.

Mhe. Rais Samia amsema kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya kuungua moto kwa shule zinazomilikiwa na Jumuiya za Dini nchini hivyo ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na  Jumuiya hizo kutafuta vyanzo vya matukio hayo na kuyadhibiti ili matukio ya kuungua moto kwa shule hizo yasijirudie.