Back to top

RAIS SAMIA AKEMEA VIONGOZI WANAOICHONGANISHA SERIKALI NA JAMII

12 April 2024
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesikitishwa na baadhi ya viongozi wasiotambua dhamana walizonazo ambao hutumia nafasi zao kuleta uchonganishi badala ya kuleta maelewano kati ya Serikali na jamii.

Rais Samia amesema hayo, wakati akizungumza katika Kumbukizi ya Miaka 40 ya kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine, akiwasisitiza viongozi kuiga mfano wa Hayati Sokoine kwani alikemea jambo hilo kwa maneno na vitendo.

Rais Samia amesema Hayati Sokoine alitumia utashi wake wa hali ya juu kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na jamii aliyoiongoza na kuiwakilisha vyema jamii ya Wamaasai.

Rais Samia amewataka viongozi wa sasa na wajao kutambua kuwa uamuzi ukifanyika ndani ya Serikali, ni wajibu watekeleze uamuzi huo kama ulivyofikiwa hata ikibidi wao wawe mfano kwa wengine kama Hayati Sokoine alivyofanya.

Kuhusu umuhimu wa elimu kama ulivyopewa kipaumbele na Hayati Sokoine, Rais Samia ametoa wito kwa wazazi kutumia vyema fursa ya miundombinu bora ya Elimu inayojengwa na Serikali kuwapeleka watoto shule.

Aidha, Rais Samia ametoa wito kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kuendelea kutunza kumbukumbu za viongozi wa Taifa na kuhakikisha habari zao zinawafikia vijana wengi zaidi kupitia njia za kisasa.

Rais Samia ametumia fursa hiyo pia kutoa pole kwa waathiriwa wote wa mafuriko na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana kuepusha madhara zaidi na kuwataka pia wananchi kusikiliza maelekezo ya tahadhari zinazotolewa.

Pia Rais Samia amesema baada ya mvua hizo na hali ya kawaida kurejea, Serikali itafanya uchunguzi wa kina kubaini sababu za mafuriko hayo ili kuepusha madhara makubwa kwa siku zijazo.