Back to top

SERIKALI INATHAMINI MCHANGO WA WANAWAKE-MAMA MWINYI

20 April 2024
Share

Mke wa Rais wa Zanzibar, Msarifu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mhe.Mama Mariam Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kutambua na kuthamini mchango wa Wanawake na kuwashirikisha katika ngazi ya maamuzi na kuendeleza maendeleo nchini.

Mama Mariam Mwinyi amesema hayo katika hafla ya Uwezeshaji na Ushirikishwaji Wanawake kiuchumi kwa Zanzibar kupitia program ya Mwanamke Shujaa ilioandaliwa na kampuni ya Coca Cola Kwanza kwa kushirikiana na Oryx Gas Tanzania, Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Wakala wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar (ZEEA) katika viwanja vya Maisara , Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 20 Aprili 2024.

Aidha Mama Mariam Mwinyi ameeleza kuwa Serikali inayoongozwa na  Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi inatambua na kuenzi mchango mkubwa unaofanywa na wajasiriamali Wanawake ikiwemo Mamalishe ambao ni kundi kubwa la Wanawake waliojiajiri  kutoa huduma ya vyakula nchini.

Mama Mariam Mwinyi ametoa rai kwa mashirika na asasi mbalimbali za kiraia kuendeleza utaratibu wa ushirikishwaji na uwezeshaji Wanawake kiuchumi katika kufikia malengo ya maendeleo ya jamii .