Back to top

TANAPA yaanza uhakiki wa mipaka ya mapori ya hifadhi Kagera

26 August 2018
Share

Shirika la hifadhi za taifa Tanzania TANAPA limeaanza kuainisha mipaka ya mapori ya akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika yaliyo katika mchakato wa kuanzishwa kuwa hifadhi za taifa ikiwa ni maagizo ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Mkurugenzi wa utawala na rasilimali watu kutoka TANAPA Witness Shoo akiongea kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa shirika la hifadhi za taifa Tanzania TANAPA Dkt. Allan Kijazi kwenye ziara ya naibu waziri wa maliasili na utalii Mhe. Japhet Hasunga kuangalia hatua zilizofikiwa katika uanzishwaji wa hifadhi hizo amesema changamoto ya barabara imepewa kipaumbele na magreda kwaajili ya kufungua barabara za utalii kwenye mapori hayo yameandaliwa ili yaanze kazi mara moja.

Kwa upande wake naibu waziri wa maliasili na utalii Mhe. Japhet Hasunga amesema kupandishwa hadhi kwa mapori hayo kuwa hifadhi za taifa ni hatua za kimkakati ya kuuingiza mkoa wa Kagera katika mpango mkubwa wa kitaifa wa kutangaza utalii wa Tanzania na kuongeza ushirikiano na nchi za afrika mashariki na pia utalii wa mikutano.

Naibu waziri wa maliasili na utalii Mhe. Japhet Hasunga pia ametembelea baadhi ya maeneo yanayofaa kuingizwa kwenye vivutio vya utalii ikiwemo daraja la Kyaka katika mto Kagera kata ya Bulifani lililojengwa na jeshi la wananchi wa Tanzania enzi za vita ya Uganda na Tanzania mwaka 1978 na pia magofu ya kanisa katoliki Kyaka ambalo lilipigwa na bomu na majeshi ya Nduli Idd Amini wakati wa vita hiyo.