Tanzania imetajwa kuwa nchi ya pili katika nchi za Afrika kwa kuwa na asilimia 52 ya watu wanaoishi kwenye maeneo hatarishi yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa wa kichocho,baada ya nigeria ambayo inaongoza kwa kuwa na idadi ya watu milioni 29 wanaougua ugonjwa huo.
Takwimu hizo zimetolewa na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo kikuu Katoliki cha Sayansi za afya na tiba Bugando (CUHAS) mkoani Mwanza Dk. Humphrey Mazigo katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa maabara kutoka wilaya mbili za Ilemela na Nyamagana mkoani humo ambapo amesema kwamba wamejipanga kuhakikisha wanapunguza idadi ya watu wenye maambukizi ya ugonjwa huo.
Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) kituo cha Mwanza, Dk. Godfrey Katano,amesema lengo la kuwakutanisha wataalamu hao ni kuwajengea uwezo ili waweze kubaini kwa haraka ugonjwa wa kichocho katika hatua za awali.
Baadhi ya wataalamu wa maabara walionufaika na mafunzo hayo, wamesema tatizo la ugonjwa wa kichocho bado ni kubwa katika maeneo mengi ya kanda ya ziwa kutokana na watu wengi kufika katika vituo vya afya kupata huduma huku wakidai mafunzo hayo yatawasaidia zaidi kuendelea kupambana na ugonjwa huo unaosababishwa na minyoo ya kichocho.
taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (nimr) kituo cha mwanza imekuja na mradi wa uendelevu wa kudhibiti ugonjwa wa kichocho katika wilaya za ilemela na nyamagana mkoani mwanza ili kupunguza idadi ya watu wanaosihi na ugonjwa huo hususani wale wanaoishi mwambao wa ziwa victoria.