Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Arusha unaotarajiwa kutumika kwa ajili ya Fainali za AFCON 2027 unaendelea vizuri licha ya mvua kubwa zinazonyesha na sasa umefikia 16% za ujenzi.
Msigwa amesema hayo leo Desemba 21, 2024 wakati wa ziara yake ya mara kwa mara ya kukagua maendeleo ya Mradi wa ujenzi wa uwanja huo unaojengwa katika kata ya Olmoti jijini Arusha.
Aidha, Msigwa amesema mradi huo wa ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Arusha utagharimu shilingi Bilioni 286 mpaka kukamilika kwake na Mheshimiwa Rais Samia ameshatoa maelekezo na fedha zinatoka kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Msigwa amesema hivi karibuni atatoa taarifa rasmi kuhusu ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Dodoma.