Back to top

ULEGA AGAWA MADUME YA NG’OMBE KWA WAFUGAJI MSOMERA

15 September 2024
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, amekabidhi  madume bora ya ng’ombe wa nyama 20 kwa vikundi vya wafugaji wa Kijiji cha Msomera ili wasaidie  kuzalisha kizazi chenye uwezo wa kutoa nyama nyingi zaidi ya wale wa asili waliopo hapa nchini. 

Waziri Ulega amekabidhi ng’ombe hao wakati wa hafla fupi ya kukabidhi madume bora ya ng’ombe wa nyama kwa vikundi vya wafugaji iliyofanyika katika kijiji cha Msomera,wilayani Handeni, mkoani Tanga.

“Tukio hili ni kutimiza mpango wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wa kuleta mabadiliko kwenye sekta ya mifugo kupitia kuboresha mbari za mifugo kwa njia ya uhimilishaji na kuwapatia wafugaji madume bora”, amesema
 
Amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya ng’ombe milioni 36.6 na kati ya hao, asilimia 97 ni ng’ombe wa asili, hivyo, sehemu kubwa ya uzalishaji wa nyama na maziwa hapa nchini unategemea zaidi ng’ombe wa asili. 
 
“Ng’ombe wetu wa asili wana uwezo wa kustahimili magonjwa na hali ya mazingira ya maeneo mengi ya Tanzania. Hata hivyo pamoja na sifa hizo, ng’ombe hawa wana uzalishaji mdogo wa nyama na maziwa. Ili kuongeza uzalishaji wa nyama na maziwa, mbinu mojawapo ni kuzalisha mifugo chotara na kuboresha mazingira ya utunzaji ikiwemo lishe. Ng’ombe wa asili wana uwezo wa kuzalisha nyama kilo 80 hadi 120 lakini wakiboreshwa wanakuwa na uwezo wa kuzalisha kilo 150 hadi 200”, amefafanua

Waziri Ulega ameongeza kwa kusema kuwa kufuatia juhudi za Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan za kutafuta masoko ya nje, soko la bidhaa ikiwemo nyama kutoka Tanzania limeongezeka kwa haraka. Mfano mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 10,415 mwaka 2021/2022 zenye thamani ya USD milioni 42.5 hadi tani 14,701.10 zenye thamani ya USD milioni 61.4 katika mwaka wa fedha 2022/2023. 

“Ili soko liwe endelevu na linalozingatia ubora wa nyama Wizara inachukua hatua za kuboresha mifugo, lishe, upatikanaji wa maji na afya ya mifugo ili kuongeza uzalishaji na ubora wa nyama ikiwemo kuhakikisha kuwa wafugaji wanapata mbegu bora”, amebainisha
 
Halikadhalika, amebainisha kuwa katika mwaka fedha wa 2023/2024 Wizara imenunua jumla ya madume 200 aina ya Boran yenye thamani ya TSh. milioni 511.2ambapo Kijiji cha Wafugaji cha Msomera kimepatiwa madume 20. 
 
Vilevile, amesema kuwa katika mwaka 2024/2025 Wizara imepanga kununua madume 66 ya nyama aina ya Brahman kutoka nje ya nchi yenye thamani ya TSh. milioni 990 ambayo yatakopeshwa kwa wafugaji kwa mkopo wa miaka 2 bila riba kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB). Utaratibu wa kuwakopesha wafugaji unafanyika ili zoezi hili liwe endelevu kwa fedha hizo kununulia madume mengine.
 

Pia Waziri Ulega amesema Wizara yake inawahamasisha wafugaji wote nchini kuachana na ufugaji wa mazoea na kufuga kibiashara. Moja ya hatua muhimu ya kuelekea kufuga kibiashara ni kuwa na mbegu bora za mifugo zenye uwezo wa kuzalisha mazao mengi. Serikali inatoa madume haya ili yawe hamasa kwa wafugaji kuendelea kununua mbegu bora baada ya kuona matokeo mazuri ya ndama wanaotokana na madume haya. 
 
Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa Kijiji cha Msomera kinakuwa kijiji cha mfano cha wafugaji. Serikali itahakikisha kuwa mahitaji yote muhimu kwa ajili ya mifugo yakiwemo majosho, minada, vituo vya kukusanyia maziwa, machinjio, malisho na maji vinakuwepo Msomera.