
Wananchi wa Kata ya Mnyawa na Nachunyu, Wilaya ya Tandaimba mkoani Mtwara, wameiomba serikali kuwaongezea nguvu ya kifedha ,ili waweze kukamilisha ujenzi wa vituo viwili vya afya, ili kuondokana na kero ya kutembea umbali mrefu unaopelekea wanawake wajawazito kujifungulia njiani.
Wananchi hao wametoa kauli hiyo wakati Benki ya NMB ikikabidhi bati 400 kwa kata hizo mbili ,zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 15, ili kusaidia ujenzi wa viituo hivyo vya afya.
Wameiomba serikali kuweka nguvu ili vituo hivyo viweze kukamilika na kuondokana na kero ya kutafuta huduma za afya ambayo inawaathiri kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wake Meneja wa NMB, Kanda ya Kusini, Janeth Shango, amesema Benki ya NMB imekuwa ikitoa misaada katika sekta hiyo, lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora ,ili waweze kufanya kazi za kiuchumi na kujiongezea kipato.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Tandaimba, Canal Patrick Sawala, ameishukuru Benki ya NMB kwa msaada huo, na kuahidi serikali itaendelea kuchangia ujenzi wa kituo hicho cha afya ili kiweze kukamilika kwa wakati na kuwaondolea adha ya huduma ya afya.