Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amezitaka nchi za Afrika wazalishaji wa madini mkakati kuweka usimamizi madhubuti wa rasilimali hizo ili zisaidie kukuza uchumi wa Afrika kwa kuhakikisha unakuwepo mkakakati imara wa kuongeza thamani madini hayo katika nchi wazalishaji.
Mh. Mavunde ameyasema hayo, alipokuwa akitoa hotuba yake wakati akishiriki Mkutano wa 13 wa Utajiri wa Madini Jijini Kampala, nchini Uganda.
"Kipekee naomba nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni kwa uamuzi wake thabiti wa hivi karibuni wa kukataza usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi. Hii ni hatua muhimu sana kwa maendeleo ya sekta ya madini na wananchi wa Jamhuri ya Uganda"
"Sisi Tanzania, tulishafanya uamuzi huo wa kukataza usafirishaji wa madini ghafi nje chini ya uongizi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumetamka bayana kwamba mwekezaji yeyote atayehitaji kuwekeza kwenye uchimbaji wa madini mkakati ni sharti aoneshe mpango kabambe wa uongezaji thamani nchini Tanzania", alisisitiza Mhe. Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde alieleza kwamba, sekta ya madini imeendelea kukua na kufanya vizuri ambapo kwa mwaka 2023, mchango wake kwenye pato la taifa ulifikia asilimia 9. Pia, asilimia 56.2 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote nje ya Nchi yalitokana na sekta ya madini, ambapo ilikadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 3.5.
Vilevile, Mhe. Mavunde alieleza kwamba kwa upande wa maduhuli, asilimia 60 huchangiwa na wachimbaji wakubwa na asilimia 40 hutokana na wachimbaji wadogo. Hali hiyo imeifanya Serikali ya Tanzania kuendelea kuweka mkazo katika kuwasimamia na kuwaongoza wachimbaji wadogo ili wazalishe kwa tija na kuongeza mchango wao kwenye uchumi wa Nchi.
Pia, Waziri Mavunde alieleza kwamba ili Nchi iweze kunufaika na madini mkakati ni lazima iwekeze fedha nyingi kwenye utafiti ili kufahamu kiasi cha madini hayo kilichopo na kuvutia wawekezaji. Alieleza kuwa katika hilo, Tanzania tayari imekuja na Mpango wa Vision 2030 wenye lengo la kuongeza eneo la utafiti wa kina kwa kurusha ndege kutoka asilimia 16 ya sasa na kufikia asilimia 50 ifikapo Mwaka 2030.
Ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania imepiga hatua katika kuendeleza sekta ya madini ukilinganisha na Uganda, na kupelekea Mhe. Mavunde kueleza wazi kuwa yupo tayari kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushirikiana na kubadilishana uzoefu na Uganda ili waweze kunufaika na rasilimali madini iliyopo nchini kwao.
Akihitimisha hotuba yake, Waziri Mavunde alisisitiza kwamba, Nchi za Afrika ili ziweze kunufaika na fursa ya kuongezeka kwa mahitaji ya madini mkakati duniani kama graphite, nikeli na cobalt ni lazima ziweke mikakati ya pamoja ya kuhakikisha zinanufaika na uchimbaji na uongezaji wa thamani madini hayo ndani ya nchi zao ili kulinda ajira, kuongeza mapato na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.
Awali, katika mkutano huo akitoa hotuba ya sekta ya madini, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Jamhuri ya Uganda, Mhe.Dkt. Ruth Ssentamu alibainisha kwamba Uganda imejipanga kuona sekta ya madini hususan madini mkakati yananufaisha Taifa, na kwamba wapo tayari si tu kujifunza kutoka Tanzania ambao wamepiga hatua kubwa kwenye sekta ya madini bali pia kushawishi uwekezaji wa fedha nyingi kwenye utafiti ili kuongeza ufanisi wa sekta ya madini ambayo kwa zaidi ya asilimia 80 imejumuisha wachimbaji wadogo.