Waziri wa ujenzi uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Isaac Kamwelwe amewaagiza wakurugenzi wa mamlaka ya viwanja vya ndege nchini TAA,mkurugenzi wa shirika la ndege nchini ATCL na mkurugenzi wa mamlaka ya usafiri wa anga TCAA kufika mkoani Iringa kukagua uwanja wa ndege wa Iringa maarufu uwanja wa Nduli ili kuona uwezekano wa ndege kubwa kuanza kutua kwenye uwanja huo.
Mhandisi waziri Kamwelwe ametoa agizo hilo mjini Iringa baada ya kukagua na kujionea ukarabati wa njia ya kurukia ndege kwenye kiwanja hicho ambapo amesema ukarabati huo uliolenga kuwezesha ndege kubwa kutua kwenye kiwanja hicho umekamilika.
Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha mipango TANROADS Mhandisi Motta Kyando amesema ukarabati uliofanyika kwenye kiwanja hicho ni katika kipande cha mita 250 eneo ambalo TANROADS na mamlaka ya viwanja vya Ndege walikubaliana kufanya ukarabati.
Pamoja na ukarabati huo kiwanja cha Ndege cha Iringa ni moja ya miradi inayotegemewa kutekelezwa kupitia mradi wa REGRO unaofadhiliwa na benki ya dunia ambapo kiwanja hicho kinatarajiwa kupanuliwa kwaajili ya kutua ndege kubwa sambamba na ujenzi wa barabara ya Iringa hadi Msembe katika hifadhi ya taifa ya Ruaha zaidi ya kilometa 100.