Back to top

Wafugaji wanaolisha mifugo katika mashamba ya wakulima kukamatwa.

03 July 2022
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack kuhakikisha anawakamata Wafugaji wote wanaopiga Wakulima na kulisha mifugo yao katika mashamba yenye mazao.

Ndaki ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua migogoro ya Wafugaji na Wakulima aliyoifanya katika Wilaya za Kilwa na Liwale, mkoani Lindi.

Amesema wafugaji wengi hasa wanaohamahama kutafuta malisho ndio wanaolalamikiwa na wakulima kuwa wao  ndio chanzo cha vurugu,wanawapiga  wakulima na kulisha mifugo yao kwa ubabe katika mashamba ya wakulima hao.

Ameongeza kuwa vitendo vya ubabe vinavyofanywa na baadhi ya wafugaji havikubaliki, huku akisisitiza kuwa nchi haiwezi kuwa na jamii ya namna hiyo, na hivyo wale wote wanaofanya vitendo hivyo hawatavumiliwa.

"Sasa Mkuu wa Mkoa na timu yako naomba  wale wote wanaopiga na kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima wakamatwe kuanzia leo hii wawekwe ndani na wafunguliwe mashtaka ili sheria ichukue mkondo wake," amesema Ndaki

Kufuatia maelekezo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack alichukua hatua za haraka na kuwaelekeza  wakuu wa vituo vya Polisi katika Wilaya ya Kilwa na Liwale kuwakamata wafugaji waliowapiga wakulima na apatiwe taarifa ya utekelezaji wake haraka.

"Yupo kijana alimpiga diwani hapa Kata ya Kimambi na amemlipa laki tatu na nusu (350, 000), nasema hiyo ni dharau na haikubaliki, nakuagiza OCD upo hapa nataka uondoke na huyo aliyemlipa diwani, na wale wote wanaohusika na vitendo hivyo wakamatwe leo ," amesisitiza

Ameongeza kwa kusema kuwa wafugaji wote walioingia bila utaratibu mkoani humo waanze kuondoka wenyewe kabla hawajaanza kushughulikiwa kwa sababu wao ndio chanzo cha vurugu.

"Afisa Mifugo na Mtendaji wa Kata nataka kuona wafugaji wote walioingia kinyemela wanaanza kuondoka, na wafugaji wengine mnaobaki mkiendekeza vitendo hivi nataka niwahakikishie nitawaondoa mmoja baada ya mwingine," amefafanua

Mmoja wa Wafugaji Wilayani Kilwa, Kidole Hababa alisema ili vitendo hivyo viweze kukomeshwa ni muhimu Serikali ikawaita Wazee wa  Wafugaji ili washirikiane nao kwa sababu wazee hao wanawafahamu vijana wanaofanya vitendo hivyo watatumia njia zao za kimila kuwawajibisha.

Aidha, katika hatua nyingi, Waziri Ndaki amewataka Wafugaji kushiriki kikamilifu katika zoezi la kusajili mifugo yao huku akiwahimiza kuanza kumiliki maeneo yao ya kufugia akiamini kuwa wakifanya hivyo itasaidia kupunguza migogoro kwa kiasi kikubwa.

Halikadhalika alitumia fursa hiyo pia kuwataka Watendaji wa Kata na Wenyekiti wa vijiji kujitafakari kwa sababu baadhi yao wanalalamikiwa kuwa sio waadilifu na kuwa ni sehemu ya migogoro hiyo.