Back to top

Wakazi zaidi ya 10,000 kunufaika na maji Muheza

17 July 2018
Share

Wakazi zaidi ya 10,000 waliopo kata za Mkanyageni,Lusanga na makao makuu ya wilaya ya Muheza wanatarajiwa kuanza kunufaikia na maji safi na salama kufuatia mradi mkubwa wa maji kutoka eneo la Pongwe Jijini Tanga hadi wilayani humo uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.5 baada ya wataalam wa ujenzi wa miundombinu kuanza kutandaza Mabomba.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo katika eneo la Mkanyageni wilayani Muheza,msimamizi wa mradi huo kutoka mamlaka ya maji safi na taka Jijini Tanga Mhandisi Shabani Rashid amesema hadi ifikapo mwezi Februari mwakani mradi huo utakuwa umekamilika.

Naye Mkandarasi wa mradi huo wa kampuni ya ujenzi ya COBERG Stephen Lucas amesema hivi sasa wameanza kujenga Tanki kubwa  katika eneo la Mkanyageni litakalo kuwa na ujazo wa lita laki 7 ili wakazi wa eneo hilo waanze kunufaika kabla mradi huo haujafika makao makuu ya wilaya ya Muheza.

Kufuatia hatua hiyo mbunge wa jimbo la Muheza  Mheshimiwa Balozi Adad Rajab amewaagiza wataalam wa ujenzi wa miundo mbinu kwa kushirikiana na mkandarasi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa muda uliowekwa.