Back to top

Wakulima wa Korosho Horohoro Tanga walia na ucheleweshaji wa Pembejeo

02 August 2018
Share

Uchelewashwaji wa pembejeo za kilimo katika kijiji cha Horohoro kilichopo halmashauri ya wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga, kimewachukiza wakulima wa zao la Korosho, mkoani humo  huku wakisema kucheleweshwa kwa pembejeo hizo kunaweza kupelekea kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo katika msimu wa mwaka 2018/ 2019.
 
Wakizungumza na ITV  baadhi ya wakulima hao ambao wanajishughulisha pia na uoteshaji wa miche ya mikorosho, wamesema kucheleweshwa kwa pembejeo za kilimo, mikorosho mingi wanashindwa kuihudumia kutokana na ukosefu wa pembejeo hizo kutowafikia kwa wakati.
 
 Kufuatia uchelewashaji wa pembejeo hizo, bodi ya Korosho Tanzania CBT inapeleka pembejeo za salfa ya unga pamoja na viwatilifu vya maji kwa ajili ya kuanza kuvisambaza  katika wilaya za Mkinga, Muheza, Pangani na Korogwe, huku wakulima wa zao la Korosho wakiombwa kutumia pembejeo za serikali zinazosambazwa kwa bei nafuu ya shilingi elfu 32 tu kwa salfa ya unga na elfu 14 kwa dawa za maji.