Kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini Sudan, wanafunzi 150 wa udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Sayansi na Teknolojia (UMST) cha Khartoum nchini humo wamehamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kukamilisha mwaka wao wa mwisho wa masomo.
Akitoa taarifa hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema wanafunzi hao wapo mwaka wa tano wa shahada ya kwanza ya utabibu, ambapo katika mwaka huo, mafunzo hufanyika kwa vitendo zaidi, hivyo madaktari hao watafanya mzunguko katika idara mbalimbali ikiwemo idara ya upasuaji chini ya usimamizi wa madaktari bingwa.