Wananchi zaidi ya 700 wa vijiji viwili vya Koresa na Uchira wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wameendelea kukosa huduma ya maji kwa zaidi ya wiki moja kwa kile kinachodaiwa ni mvutano baina ya bodi mbili za maji zinazohudumia wananchi hao.
Wananchi wa vijiji hivyo wamesema hali ni mbaya kutokana na wanawake kuhangaika na ndoo za maji kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji safi na salama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya jumuiya ya watumia Uchira Bw.Lazaro Mfinanga amekiri kuwapo kwa tatizo hilo ambalo anadai linasababishwa na bodi ya maji Kirua Kahe Mtiririko kuhujumu jumuiya ya watumia maji Uchira hali ambayo inasababisha adha kubwa kwa wananchi.
ITV imefika katika ofisi ya maji Kirua Kahe Mtiririko na kukutana na Meneja wa bodi hiyo bw.Mambeya Mshana ambaye amesema tatizo la ukosefu wa maji katika vijiji hivyo linasabaishwa na uharibifu wa miundombinu kwenye matanki yanayosambaza maji kwenye vijiji hivyo na kwamba tayari mafundi wameanza matengenezo.