![](https://www.itv.co.tz/sites/default/files/styles/large/public/field/image/tanesco.jpg?itok=CL0bqfqb)
Waziri wa nishati Dkt. Medard Kalemani amewaonya baadhi ya watu wanaohujumu miundombinu ya umeme pamoja na vishoka wanaojifanya mafundi wa mradi wa umeme vijijini REA kwa kuwatoza wananchi gharama kubwa za kuwaunganishia umeme majumbani mwao tofauti na shilingi 27,000 kwamba siku zao zinahesabika kwani wakikamatwa mwisho wao utakuwa ni kifungo magerezani.
Dkt. Kalemani ametoa onyo hilo wakati akiwasha umeme wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza katika vijiji vya Ibindo na Ngula vilivyopo jimbo la Sumve wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, ambapo amemuagiza mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga kutoruhusu mtu yeyote kuhujumu miundombinu ya umeme, kwani serikali imetumia fedha nyingi kugharimia miradi ya nishati ya umeme, ukiwemo umeme wa REA ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi wa maeneo ya vijijini