![](https://www.itv.co.tz/sites/default/files/styles/large/public/field/image/QWA.jpg?itok=LxTJSP-2)
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Tanzania Dkt. Ntuli Kaporogwe anatarajiwa kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye uchaguzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati, na Kusini (ECSA – HC).
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika leo Februari 11, 2025 kwenye Mkutano Mkuu wa 74 Mawaziri wa Afya wa Jumuiya hiyo unaoendelea kufanyika Jijini Lilongwe, Malawi.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakati akimnadi Dkt. Ntuli amesema kuwa, ana uzoefu mkubwa katika utawala wa afya, maendeleo ya sera pamoja na uhamasishaji wa rasilimali na uimarishaji wa mifumo hasa ndani ya Wizara ya Afya ya Tanzania, uzoefu huu unamwezesha kuendeleza malengo ya ECSA-HC, ikiwa ni pamoja na huduma ya Afya kwa wote (Universal Health Coverage).
Amesema, Dkt. Ntuli ana rekodi iliyothibitishwa katika kupata ufadhili wa ndani na kimataifa kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa afya, hasa wakati huu ambapo ufadhili umezidi kuwa na changamoto kutokana na mabadiliko katika sera ya ufadhili wa kigeni ya Marekani.
“Akiwa Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, ameonesha uongozi wake wa kushughulikia majanga ya magonjwa ya milipuko, ikiwa ni pamoja na COVID-19, Marburg mwaka 2023, na Marburg 2025, juhudi zake zimekuwa muhimu katika kuunganisha wataalam wa afya na washirika, lakini pia kuimarisha ufuatiliaji wa mipaka kwa kushirikiana na mashirika ya ndani na Kimataifa” amesema Waziri Mhagama.
Chini ya uongozi wa Dk. Ntuli, ECSA-HC itakua tayari kuchukua jukumu kubwa katika kukabiliana na milipuko, kama taasisi ya afya ya kikanda, ECSA-HC lazima iratibu kikamilifu juhudi za kuzuia kuenea kwa magonjwa na kuimarisha usalama wa afya kwa nchi wanachama wa Jumuiya.
"Dk. Ntuli atatoa kipaumbele kwa kuendeleza miundombinu mipya ya makao makuu, kuhakikisha inakidhi matakwa ya jumuiya ya afya na kukuza ushirikiano na kuongeza ushawishi, uzoefu wake katika kusimamia miradi mikubwa ya afya utaongoza mpito huu," ameongezea Waziri Mhagama
Jumuiya ya ECSA-HC ilianzishwa mwaka 1974 na inajumuisha nchi tisa zikiwemo; Tanzania, Malawi, Kenya, Lesotho, Zambia, Zimbabwe, Mauritius, Uganda pamoja na Eswatini na inashirikiana na nchi 13 zisizo wanachama ambazi ni Botswana, Burundi, Cameroon, Eritrea, Gabon, Liberia, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Seychelles, Sudan ya Kusini, Sudan, na Somalia.
Jumuiya ina jukumu la kukuza na kuimarisha Ushirikiano wa kikanda wa kushughulikia masuala ya Afya baina ya nchi ya wanachama ikiwemo kutatua changamoto za sekta ya afya, na kupeana uzoefu wa kuboresha huduma za afya.