Back to top

Watafiti watoa taarifa ya awali samaki waliokufa Bahari ya Hindi.

22 July 2021
Share

Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania imesema uchunguzi wa awali uliofanywa juu ya samaki Kilogramu 164 waliokutwa wamekufa katika fukwe ya Bahari ya Hindi karibu na Hospitali ya Ocean Road Jijini Dar es Salaam jana umeonesha kuwa huenda samaki hao wamekufa kwa kukosa hewa ya Oksijeni kutokana na mabadiliko ya upepo baharini au kula vimelea vyenye viambata vya sumu.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania kituo cha Dar es Salaam, Dkt.Simon Juma Kangwe amesema taasisi hiyo ni miongozi mwa taasisi zilizochukua sampuli ya samaki hao kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi kubaini chanzo cha vifo vya samaki hao.

ITV imepita katika fukwe mkabala na barabara ya Barack Obama karibu na Hospitali ya Ocean Road na kukuta baadhi ya samaki waliokufa na baadhi ya wananchi wakiwaokota kwa kile walichokisema ni kwa ajili ya chakula.

Dkt.Kangwe amesema samaki hao wanaweza kusababisha madhara kuanzia magonjwa ya ngozi hadi kusababisha kifo.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano Wizara ya Mifugo na uvuvi imewataka wananchi kuendelea na biashara ya samaki na umma utajulishwa kuhusu sababu za vifo vya samaki hao uchunguzi wa maabara utakapokamilika.