Back to top

WATATU MBARONI TUHUMA WIZI MITUNGI YA GESI.

05 October 2024
Share

Jeshi la Polisi mkoani Songwe, linawashikiliwa watuhumiwa watatu ambao ni wanaume kwa tuhuma za  uvunjaji na wizi, ambapo baada ya mahojiano ya kina watuhumiwa hao wamekiri kuiba vitu mbalimbali ikiwemo mitungi ya gesi ya kupikia, katika Miji ya Vwawa na Mlowo, iliyopo wilayani Mbozi Mkoani humo.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP. Augustino Senga, amesema kwa kipindi cha mwezi Septemba, mwaka huu jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa 321 kwa tuhuma mbalimbali wakiwemo hao watuhumiwa watatu waliokutwa na vifaa vya kuvunjia pamoja na mali mbalimbali za wizi ikiwemo mitungi ya gesi ya kupikia.
 
Aidha kamanda senga katika taarifa yake amesema kwa upande wa mahakama jeshi hilo limefanikiwa kuwapandisha kizimbani watuhumiwa kumi ambapo saba wakihukumiwa miaka thelathini jela kwa kubaka ,wawili wakihukumiwa kifungo cha maisha kwa kulawiti huku mmoja akienda jela miaka nane kwa kosa la unyang’anyi.
 
Katika hatua nyingine kamanda senga amewataka wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuendelea kusalimisha silaha zao huku akitoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa za uhalifu .