
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa, amewataka wakuu wa Wilaya na Waganga wakuu wa mikoa yote nchini, wasimamie maadili kwa watumishi wa sekta ya afya ili fedha zinazotolewa kwenye sekta hiyo, ziendane na ubora wa huduma zinazotolewa kwa Watanzania.
Amesema kuwa Mhe.Rais Samia ameendelea kuhakikisha anatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya, ununuzi wa dawa na vifaa tiba, hivyo dhamira yake hiyo ni lazima iendane na ubora wa huduma zinazotolewa na watumishi katika sekta ya afya.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo, wakati akizungumza na viongozi wa Serikali wa mkoa wa Ruvuma, kwenye ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Songea.
Amewaagiza wakuu wa Wilaya kusimamia upatikanaji wa dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Busket Fund kwani Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anatoa fedha za ununuzi wa dawa.
Katika Hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa wilaya kwa kushirikiana na Wakurugenzi na Maafisa Elimu, wasimamie dhamira ya Mheshimiwa Rais. Dkt. Samia ya kutoa elimu bila malipo kaunzia darasa la awali hadi kidato cha sita kwa kutembelea katika shule na kukagua fomu za kujiunga na shule na kujiridhisha hakuna michango ya hovyo.
Ameagiza kuwepo na usimamizi wa shughuli za ustawi wa jamii ikiwemo masuala ya kiuchumi na kwa wafanyabiashara wadogo, wakati na wa kubwa.