Back to top

WAVUVI WATAKIWA KUFANYA UVUVI ENDELEVU

06 July 2023
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega, amewataka Wavuvi Wilayani Kilombero kujiepusha na matumizi ya zana haramu kama vile nyavu za nailoni na makokolo kwani ni hatari kwa maendeleo ya uvuvi.

Mhe.Ulega ameyasema hayo wakati akiongea na Wavuvi wa Kivukoni, Ifakara alipofanya ziara Wilayani Kilombero, Mkoa wa Morogoro.

Amesema matumizi ya zana haramu yamekuwa ni chanzo cha uharibifu wa mazalia ya samaki na kupelekea rasilimali hiyo kupungua na kama matumizi hayo yakiendelea yatapelekea athari kubwa kwa sekta ya uvuvi nchini.

Aidha, ameielekeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) kushirikiana na Serikali za vijiji Wilayani humo katika kuelimisha Wavuvi na Wananchi kwa ujumla juu ya umuhimu wa uvuvi endelevu ikiwemo ulinzi wa mazalia ya samaki.

Halikadhalika, Mhe.Ulega amewaeleza wavuvi hao pia kuwa na shughuli mbadala ili kujiongezea kipato ikiwemo kufanya ufugaji wa samaki katika Mto Kilombero.

Ameongeza kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na wavuvi ikiwemo kuwawezesha zana na utaalam mbalimbali ili shughuli zao ziweze kuwa na tija zaidi.