Back to top

Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana asisitiza ushirikiano katika Utalii.

15 December 2022
Share

Wataalamu katika sekta ya Maliasili na Utalii kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wametakiwa kuongeza kasi katika kubuni mazao mapya ya Utalii, uhifadhi na kutangaza vivutio vya Utalii ili kuhakikisha maeneo mengi ya Malikale  yanaingia katika hadhi ya ushindani wa Kimataifa.

Aidha, amewataka wataalam hao waendelee kuishirikisha jamii katika masuala ya Uhifadhi endelevu na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kulinda,kutunza na kuendelea kutunza maeneo ya hifadhi.

Waziri wa Maliasili na Utaliii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito hu oleo jijini Dodoma alipokuwa akifungua rasmi kikao kazi cha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika sekta ya Maliasili na Utalii, katika ngazi ya Mawaziri.

Waziri Balozi Dkt. Chana amesema kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wamefanya kazi kubwa ya kuinua na kuitangaza sekta ya Maliasli na Utalii  kupitia Filamu ya The Royal Tour, hivyo ni mashirikiano ya wataalam wa pande zote mbili yataendeleza jitihaza hizo.

“Ni wazi kuwa programu ya The Royal Rour  imekuwa na matokeo chanya katika  sekta ya utalii kwa pande zote mbili za Muungano kutokana na idadi ya watalii walioongeza tangu kuzinduliwa kwake pamoja na kuongezeka kwa wawekezaji walionesha nia ya kuja kuwekeza Tanzania”. Amesema Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana.

Naye Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe. Simai M. Said licha ya kuwapongeza wataalam wa pande mbili za Serikali ya Muungano kwa kuamua kukutana, amewataka kuhakikisha wanaimarisha mashirikiano katika kutangaza vivutio vya Utalii vya pande zote mbili (SMT na SMZ) ili kuongeza idadi ya watalii kwenye vivutio vya Utalii nchini.

Mhe. Simai amepongeza juhudi zinazofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii nchini huku Waziri wa wa Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Shamata S. Khamisi, akisisitiza kuwa ushirikiano uliopo utaendelea kuimarisha Sekta ya Maliasili hususani uhifadhi wa misitu katika pande zote mbili za Muungano.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na Mawaziri hao watatu na Wataalam wa Maliasili na Utalii kutoka Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na mambo mengine kimejadili na kuazimia mambo kadhaa  kwa lengo la kuimarisha  ushirikiano katika sekta ya Maliasili na Utalii.