
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa, ametangaza ratiba ya maziko ya Rais mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi, itakayoanza leo Machi 01, 2024.
.
Waziri Mkuu amesema mwili utaondoka nyumbani kwa Hayati Mwinyi saa 5:30 Asubuhi, kuelekea Msikiti Mkuu wa BAKWATA Kinondoni ambapo Sheikh Dkt. Abubakar Bin Zuber Bin Ali, ataongoza swala ya Ijumaa na taratibu zote za kidini.
.
Saa 8:00 Mchana, mwili wa Hayati Ali Hassan Mwinyi, utaelekea Uwanja wa Uhuru na kwamba kuanzia saa 8:30 mchana ni dua na maombi kutoka kwa Viongozi wa Dini, pamoja na Viongozi mbalimbali na Wananchi kutoa heshima za mwisho.
.
Saa 11:00 jioni mwili wa Hayati Ali Hassan Mwinyi, utaondolewa uwanja wa Uhuru kuelekea uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere, na saa 11:30 Jioni Wananchi wa Zanzibar na maeneo mengine ya Unguja wataupokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume.