Kwa mara ya kwanza timu ya madaktari katika Hospitali ya Ganga Ram huko Delhi, India imefanikiwa kumpandikiza mikono mchoraji ambaye alipoteza mikono yote miwili kwenye ajali ya treni mnamo 2020.
Upasuaji huo ulitajwa kuwa mgumu sana, na ulidumu kwa saa 12 huku ukibatizwa jina la 'upasuaji wa muujiza' na vyombo vingi vya habari nchini India .
Upasuaji ulihusisha kuunganisha kila mshipa wa damu, misuli, na neva kati ya mikono ya mtoaji na mikono ya mpokeaji.
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Times Now, mikono hiyo ilitolewa na mwanamke aitwaye Meena Mehta, ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Utawala wa Shule maarufu Kusini mwa Delhi na mwanamke huyo aliahidi kutoa baadhi ya viungo vyake kwa wenye uhitaji baada ya kifo chake.
Hadi sasa, figo zake, ini, na sehemu ya macho ambazo zimebadilisha maisha ya watu watatu na sasa, mikono yake imetolewa kwa mchoraji.