Maofisa, Wakaguzi na Askari wa Makao Makuu Zanzibar na Mkoa wa Mjini Magharibi, wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu na kutoa huduma bora wanapokuwa katika majukumu yao ya kipolisi.
Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad, ambapo amewasisitiza Maofisa hao kuwa kufanya kazi kwa uadilifu kutapelekea kutenda haki na kupatikana kwa usawa.
Amesema haki inapotendeka mashirikiano ya Jeshi la Polisi na Jamii yataimarika na kupelekea kupunguza ama kuondoa kabisa uhalifu na wahalifu.
CP Hamad amesema Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinaendelea kuboresha mazingira mazuri ya kufanyia kazi na kuimarisha maslahi ya Askari na uwepo wa vitendea kazi, huku akisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameridhishwa na utendaji kazi wa Askari na hasa kupungua kwa malalamiko juu ya suala la rushwa.