Back to top

WAZALISHAJI WA VYAKULA VYA MIFUGO WAASWA KUZINGATIA UBORA

04 October 2024
Share

Wazalishaji wa vyakula vya Mifugo nchini wameaswa kuzingatia ubora wanapozalisha vyakula vya Mifugo ili kulinda afya za watumiaji wa mazao yatokanayo na Mifugo, kuongeza ustawi wa Mifugo, kuongezeka kwa uzalishaji Mifugo pamoja na kukuza vipato vya wafugaji.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Bw. Furaha Kabuje alipokuwa akifanya ukaguzi wa vyakula vya Mifugo kwa wazalishaji na wauzaji wa vyakula hivyo kwa Wilaya za Mkoa wa Dar Es Salaam (Ubungo, Temeke, kigamboni na Ilala) kuanzia kwa lengo la kufuatilia na kujiridhisha uzalishwaji wa   vyakula hivyo kama vinafuata taratibu zilizowekwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

“Tunafanya ukaguzi huu kuangalia uzalishaji, kuona kazi zinazofanyika, kukagua vibali vya uzalishaji sambamba na kujiridhisha vyakula mnavyozalisha kama vimehakikiwa ubora na Maabara kuu ya Veterinari kwa lengo la kulinda afya za watumiaji wa mazao ya Mifugo.”

“Tunachukua sampuli za vyakula kwa wazalishaji pamoja na wauzaji tunakwenda kuzipima Maabara Kuu ya Veterinari. Kwa wale watakaobainika kufanya udanganyifu kwa kuzalisha vyakula visivyokidhi ubora tutawachukulia hatu kali kwa mujibu wa sheria.” Amesema Bw. Kabuje

Mmoja wa wamiliki wa kiwanda cha uzalishaji wa chakula cha Mifugo cha HUATANG INVESTIMENT GROUP kilichopo Chanika Bi. Chen Meng Yan alisema kuwa kipaumbele chake kikubwa ni ubora wa chakula cha Mifugo na mara zote amekuwa akihakikisha chakula kinapimwa ubora kabla hakijakwenda sokoni ili kujihakikishia ubora.

“Hatuwezi kuzalisha chakula chenye kiwango cha chini maana kampuni yetu itakufa na hata wafanyanyakazi wetu watapoteza kazi zao, vilevile hatutaki kupata hasara ndio maana tunazingatia ubora.” Amesema Bi. Chen

Bw. Adili Krisoston muuzaji wa vyakula vya Mifugo ameishukuru Serikali kwa kufanya ukaguzi wa vyakula hivyo mara kwa mara kwani kitendo hicho kinawahakikishia kuwa vyakula wanavyovinunua kwa wazalishaji vinakaguliwa na vinakidhi ubora kwa ustawi wa Mifugo pamoja na afya za watumiaji wa mazao ya Mifugo.