Back to top

"AFRIKA IUNGANISHE NGUVU UENDELEZAJI WA JOTOARDHI"

23 October 2024
Share

Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amesema Bara la Afrika, linapaswa kuunganisha nguvu na kushirikiana ili kuweza kuendeleza ipasavyo nishati ya Jotoardhi, ambayo ni safi na endelevu na kuondokana na nishati zisizo safi katika kuzalisha umeme ikiwemo mafuta mazito.

Dkt.Mpango amesema hayo jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Kongamano la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10), ambalo limehudhuriwa na washiriki 800 kutoka nchi 21 duniani.

Aidha, amesema kila nchi inapaswa kuwa na Taasisi maalum kwa ajili ya kusimamia  uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi na kuwa na kanuni na sheria madhubuti zitakazowezesha sekta binafsi kushiriki katika uendelezaji wa nishati hiyo.

Awali, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga alimshukuru Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kujitoa kwake katika kuendeleza Sekta ya Nishati na uongozi wake unaotoa  Dira katika kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu Sekta.

Vilevile ameziasa nchi zenye Nishati ya Jotoardhi kufanya mazungumzo ya kimkakati na Taasisi za kifedha ikiwemo Mabenki ili kupata fedha za kuendeleza nishati hiyo kutokana kuhitaji fedha nyingi katika uendelezaji wake badala ya kutegemea bajeti za Serikali pekee.

Amesema mipango ya Tanzania ni kuwa na umeme wa kiasi cha zaidi ya megawati 5000 ifikapo mwaka 2030 kutoka vyanzo mchanganyiko huku nishati jadidifu ikipewa kipaumbele ikiwemo Jotoardhi, upepo na Jua.

Ameeleza kuwa, Tanzania iliamua kwa vitendo kuendeleza nishati ya Jotoardhi kwa kuchukua hatua mbalimbali  ikiwemo kuanzisha Taasisi inayosimamia sekta husika mwaka 2014 ambayo moja ya kazi zake  ni kusimamia uendelezaji wa nishati hiyo.

Amesema tayari Tanzania imekamilisha utafiti wa awali kwenye baadhi ya maeneo matano yenye viashiria vya Jotoardhi kwenye Bonde la Ufa na sasa kuna uchorongaji unaoendelea katika eneo la Ngozi ili kuhakiki uwepo wa nishati hiyo.

Ameongeza kuwa, hatua nyingine iliyopigwa kwenye Jotoardhi nchini ni kuongezeka kwa idadi ya wataalam waliobobea katika masuala ya nishati hiyo na ununuzi wa rig itakayotumika kwa ajili ya shughuli za uchorongaji kwenye maeneo yenye mashapo ya Jotoardhi.

Amewashukuru Wadau mbalimbali wa maendeleo wa wanaoiunga mkono Tanzania kifedha na kiufundi ili kuendeleza nishati ya Jotoardhi ikiwemo Japan, Iceland na Ireland.

Katika kongamano hilo, Dkt. Mpango amewakaribisha Wawekezaji ili kuendeleza nishati ya Jotoardhi katika vyanzo mbalimbali ikiwemo Ngozi   (70MW), Kiejo-Mbaka (60MW), Songwe (kati ya 5 na 35MW), Natron (60MW) na Ruhoi (5MW).

Pia amekaribisha washiriki wa ARGeo-C10 kufanya  uwekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya madini na kufanya utalii katika vivutio mbalimbali ikiwemo Mlima Kilimanjaro, Serengeti, Ngorongoro n.k

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi  katika  Ofisi ya Rais, Capt. George Mkuchika amesema chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan sekta ya nishati imezidi kupiga hatua ambapo umeme vijijini umefika kwa takriban asilimia 98 na ifikapo Desemba mwishoni vijiji vyote vitakuwa vimesambaziwa.

Ameeleza kuwa hali hiyo ni kielelezo cha mahitaji ya umeme kuongezeka hivyo lazima uendelezaji wa vyanzo mchanganyiko vya nishati uongezeke ikiwemo Jotoardhi ambayo ikiendelezwa itaweza kuzalisha umeme wa megawati 5000.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Mafuta kutoka Kenya, James Wandayi amesema kuwa nchi hiyo tayari imepata mafanikio katika nishati ya Jotoardhi kwani kwa sasa zaidi ya asilimia 45 ya umeme nchini humo unazalishwa na Jotoardhi.

Amesema Nishati ya Jotoardhi inapaswa izidi kupigiwa chapuo barani Afrika kutokana na kuwa ni endelevu ambapo licha ya kutumika kuzalisha umeme inatumika pia kwenye sekta nyingine ikiwemo kilimo na ufugaji.

Awali, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga alimshukuru Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kujitoa kwake katika kuendeleza Sekta ya Nishati na uongozi wake unaotoa  Dira katika kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu Sekta.

Amesema Jotoardhi itawezesha azma ya Tanzania kuwa na umeme unaotokana na vyanzo mchanganyiko huku lengo likiwa ni kuzalisha kiasi cha megawati 995 kutokana na nishati hiyo ifikapo mwaka 2024 hali itakayoongeza pia usalama wa gridi ya umeme.

Amesema nishati ya Jotoardhi ni suluhisho muhimu katika utatuaji wa changamoto za upatikanaji wa nishati ya kutosha barani Afrika ambayo inaenda sambamba na mipango ya dunia katika kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.

Hafla ya ufunguzi wa Kongamano la ARGeo-C10 imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wabunge, Mabalozi wa nchi mbalimbali, Madiwani, Wadau wa Maendeleo na Watendaji kutoka Taasisi za Serikali na Binafsi.