Back to top

TSAP YAJA NA MIKAKATI YA KUINUA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI

24 October 2024
Share

Chama cha Wataalam wa Mifugo nchini (TSAP) kupitia kongamano lake la 47 linalofanyika jijini Arusha, kimeainisha mikakati mbalimbali inayolenga kuinua sekta za Mifugo na Uvuvi nchini, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha na kujadili tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalam hao kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya na Uganda.

Akizungumza wa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Mkurugenzi wa Uzalishaji na masoko ya mazao ya mifugo nchini Bw.Stephen Michael, amewaelekeza wataalam hao, kuhakikisha wanatumia kongamano hilo kujadili mikakati ya kufanya mapinduzi kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya Mifugo na samaki ili kukidhi mahitaji ya wananchi na masoko ya nje.

"Hivyo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatia mkazo kwenu wataalam muweke nguvu katika taaluma zenu ili kuongeza uzalishaji wa malisho na mbegu za malisho, vyakula bora vya mifugo na samaki, vifaranga bora vya kuku, mitamba bora ya ng’ombe wa maziwa, vifaranga bora vya samaki, maziwa na bidhaa zake pamoja na nyama na kupunguza upotevu wa mazao ya Mifugo na Uvuvi baada ya kuvunwa" Amesisitiza Bw. Michael.

Akielezea malengo ya kongamano hilo Mwenyekiti wa chama hicho Dkt.Jonas Kizima amesema kuwa mbali na kubadilishana uzoefu na teknolojia mbalimbali zinazoongeza uzalishaji wa mifugo na Samaki, kongamano hilo linalenga kuhimiza maendeleo katika sayansi ya uzalishaji na uendelezaji wa mifugo na Uvuvi nchini.

"Malengo mengine ni kuongeza ushirikiano baina ya wataalam hao na kutoa fursa kwa wadau wote wa sekta za Mifugo na Uvuvi nchini kukutana kila mwaka na kupeana matokeo mbalimbali ya tafiti waliozofanya na kushirikiana na vyama vingine vya kitaaluma ili kuongeza wigo wa utaalam katika kuhudumia sekta za Mifugo na Uvuvi nchini" Ameongeza Dkt.Kizima.

Naye Katibu Mkuu wa chama hicho Prof. George Msalya amesema kuwa chama chake na wataalam  wanakusudia kutumia jukwaa hilo kuishauri Serikali na wadau wa Sekta hizo juu ya namna ya kubadilika kutoka kwenye Ufugaji na Uvuvi wa chakula na kuwa na fikra za kibiashara ambapo ameongeza kuwa hatua hiyo itaboresha uchumi wa Wafugaji, Wavuvi na Taifa kwa ujumla.

Akielezea anayotarajia kutoka kwenye kongamano hilo, Mshiriki kutoka Chuo kikuu cha Maseno nchini Kenya Bi. Phoebe Mose amesema kuwa kongamano hilo litawasaidia kupata suluhu ya changamoto mbalimba zinazokabili sekta za Mifugo na Uvuvi  na namna wanavyoweza kubadili maisha ya kundi kubwa la wananchi walioajiriwa kupitia sekta hizo kupitia teknolojia mbalimbali zinazotumika kwenye nchi washiriki wa kongamano hilo.

Mbali na Kongamano hilo, Wataalam hao watatumia fursa hiyo kufanya mkutano mkuu wa 48 wa  wanachama wake ambapo pia watapata fursa ya kufanya shughuli za uwandani kwa baadhi ya Taasisi na wadau wa Sekta za Mifugo na Uvuvi mkoani Arusha huku wanachama wanaotoka nje ya nchi wakipata fursa ya kutembelea moja ya vivutio vya kitalii vinavyopatikana mkoani humo.