Serikali imesema kuwa imeendelea kuwajengea uwezo Wataalamu wa ndani wa kada mbalimbali nchini ikiwemo ya Ubunifu Majengo na Ukadiriaji Majenzi kwa kuwashirikisha kwenye miradi mkubwa kupitia Wizara ya Ujenzi.
Akizungumza Oktoba 29, 2024 jijini Dar es Salaam, katika Mkutano wa Tano wa mwaka wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema kuwa Serikali inaendelea kutoa hamasa kwa wataalam hao kuchangamkia fursa za kazi katika miradi mikubwa inayondelea hivi sasa nchini.
“Niipongeze Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa fursa kwa wazawa kushiriki miradi mikubwa nchini, sasa ni muhimu kwa wataalamu wetu wa ndani kufanya juhudi za makusudi za kujifunza uendelezaji wa nchi yetu kwa kutumia na Teknolojia ya kisasa ili kupata miradi mingi kama wataalamu wa nje,” amesema Mpogolo.
Aidha, Mpogolo ametoa rai kwa Kampuni za ndani kushiriki katika michakato yote ya zabuni ya miradi mikubwa ili hatimaye kujijengea uwezo wa kitaaluma na kupunguza utegemezi wa wataalam kutoka nchi za nje.
Ametoa rai kwa Bodi ya AQRB kuendelea kusimamia wataalam hao, kuendelea kutoa ushauri wa kitaalam kwa miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini ili kusaidia kupunguza malalamiko ya weledi na ujuzi na utekezaji wa miradi nchini.