Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa uwepo wa Viwanda vya kuchakata mazao ya Uvuvi kwenye mikoa inayozungukwa na Ziwa Tanganyika umekuwa chachu ya Maendeleo ya wananchi wa mikoa hiyo.
Mhe. Dkt. Kijaji amesema hayo wakati wa hafla ya ufunguzi wa kiwanda cha kuchakata samaki na dagaa wa Ziwa Tanganyika cha LIFA kilichojengwa mkoani Kigoma ambapo mbali na kuwapongeza wawekezaji hao kwa kuwawesha wananchi wa mkoa huo kupata ajira amewataka kushirikiana na Serikali kwenye ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi wa ziwa hilo ili kuwa na uendelevu wa upatikanaji wa malighafi za kuendeshea kiwanda hicho.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe. Dkt. Rashid Chuachua ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi hususan upande wa sekta ya Uvuvi kwa kuwawezesha wavuvi wa mkoa huo nyenzo na elimu inayowawezesha kufanya shughuli zao kwa mafanikio ambapo ameahidi kuendelea kushirikiana nao kwenye eneo la ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi wa Ziwa hilo kwa kadri watakavyoendelea kupokea maelekezo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho Bw. Benny Ngozi amesema kuwa kiwanda hicho kimegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 300 mpaka kukamilika kwake ambapo ameongeza kuwa hadi sasa wamefanikiwa kutoa ajira za moja kwa moja na za mzunguko kwa takribani watu 520.