Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amewakaribisha wafanyabiashara wa Czech kuwekeza nchini Tanzania, na kuzinadi fursa nyingi za uwekezaji zinazopatikana katika sekta za utalii, uchukuzi, afya, TEHAMA, nishati, madini, na elimu.
Waziri Kombo ametoa mwaliko huo wakati wa mazungumzo na wamiliki na viongozi wa kampuni kubwa za Czech alipokuwa katika ziara ya kikazi nchini humo.
Amesema Czech imepiga hatua kubwa za maendeleo katika sekta mbalimbali, hivyo Tanzania inaweza kunufaika kwa uhaulishaji wa teknolojia na mitaji na kwamba uwekezaji wa Czech utawafaidisha Watanzania kupitia ajira na ujuzi wa kiufundi.
Waziri Kombo amewahakikishia wafanyabiashara hao kwamba Tanzania iliyo katika eneo la kimkakati na yenye utajiri wa rasilimali, ni chaguo bora kwa uwekezaji.