Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amekutana na uongozi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya huduma za Afya ya nchini Korea (KOFIH) kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya Afya ikiwemo kuimarisha huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto katika mikoa ya Pwani na Dodoma.
Pia wamejadili masuala ya kuendelea kujenga uwezo kwa Maabara ya Kitaifa ya Afya ya Umma juu ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza, mpango wa kiufundi wa usimamizi wa hospitali pamoja na ukarabati na ujenzi wa wodi maalum za watoto wachanga wagonjwa (NICU).
Katika kikao hicho, Waziri Mhagama amesema katika kipindi cha miaka mitano (5), Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imenufaika na ushirikiano wa pamoja na Serikali ya Korea kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Nne wa Sekta ya Afya (HSSP-IV) pamoja na Mpango Mkakati wa Tano.
"Kwa sababu hiyo, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya Korea pamoja na taasisi ya (Korea Foundation for International Healthcare, KOFIH) kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Tanzania, hususan katika sekta ya afya," amesema Waziri Mhagama