Back to top

RAIS SAMIA KUZINDUA DARAJA LA PANGANI NA BOTI ZA UVUVI

26 February 2025
Share

Wakati Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akiendelea na ziara yake mkoani Tanga ambapo pamoja na mambo mengine, anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la Ujenzi wa daraja la Mto Pangani na barabara ya Bagamoyo (Makurunge)- Saadan na Tanga- Pangani.

Kulingana na Mamlaka za serikali, Daraja la Pangani lina urefu wa Mita 525, likiwa na upana wa mita 13.55, yenye mgawanyiko wa Mita 8 kwaajili ya magari, Mita nne kwaajili ya watembea kwa miguu na Kingo imara zitakazowekwa pembezoni mwa daraja.

Mradi huu unagharimu takribani Bilioni 82 na kufikia leo umefikia asilimia 52.88 za ujenzi wake, likiwa na sifa moja kubwa ya kuunganisha kenya, Tanga pamoja na Bagamoyo na hivyo kuwa daraja na barabara muhimu katika kusisimua uchumi na maendeleo ya jamii ya pembezoni mwa miradi hii.

Kukamilika kwa daraja na barabara hiyo unganishi kutasisimua na kukuza uchumi wa Mji wa Pangani na maeneo ya jirani kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu unaotarajiwa kufikia mwishoni mwa mwaka huu pale mradi huo utakapokamilika.

Daraja la Mto Pangani na barabara zake unganishi zinazojengwa kwa kiwango cha Lami, zinatarajiwa pia kuamsha utalii katika hifadhi  ya Saadan sambamba na kurahisisha huduma ya usafirishaji wa malighafi mbalimbali hasa kwa kuzingatia kuwa Mkoa huu wa Tanga unao wakulima wanaojihusisha na kilimo cha Nazi pamoja na Mkonge.

Rais Dkt. Samia pia atazindua Boti za uvuvi na boti za Kilimo cha mwani na baadae kuzungumza na wananchi wa Wilaya ya Pangani kwenye uwanja wa Kumba, lengo likiwa ni kuboresha shughuli za uvuvi, kukuza uchumi wa buluu na kuimarisha ulinzi na rasilimali bahari.

Rais Samia pia leo Jumatano ataweka jiwe la msingi la upanuzi wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa na kuzungumza na waumini wa msikiti huo.