Back to top

RAIS SAMIA ATATUA CHANGAMOTO YA MAJI MKINGA

27 February 2025
Share

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonesha dhamira thabiti ya kutatua changamoto ya maji wilayani Mkinga kwa kuwekeza shilingi bilioni 35. 4 kwenye mradi mkubwa wa maji kutoka Mkinga na Horohoro.

Akizungumza leo Alhamisi, Februari 27, 2025, katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo, Waziri Aweso amesema kuwa, changamoto ya maji katika jimbo la Mkinga ilikuwa kilio cha muda mrefu cha wananchi, jambo lililomfanya Mbunge wa Mkinga, Dunstan Kitandula, kuibua hoja hiyo mara kwa mara bungeni.

Amesema kuwa wakati fulani mbunge huyo alitaka kushikilia bajeti ya Wizara ya Maji bungeni, lakini alimuomba kusubiri na kuahidi kutembelea jimbo hilo ili kusikiliza moja kwa moja kilio cha wananchi. 

Baada ya ziara hiyo, Waziri Aweso alimweleza Rais Samia kuhusu hali ya maji Mkinga, ambapo Rais aliamua mara moja kuwa lazima mradi mkubwa wa maji ujengwe kwa gharama yoyote ile.

"Rais Samia ulisema kwamba kwenye kutatua matatizo ya wananchi huangalii gharama, hasa suala la maji. Kutatua changamoto za wananchi kunahitaji utashi wa kisiasa, maamuzi magumu, na uthubutu, na wewe una yote haya," alisema Waziri Aweso.

Waziri Aweso amebainisha kuwa, mradi huo wa kilometa 90 kutoka Zigi hadi Mkinga ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa kwa fedha za ndani badala ya kutegemea wafadhili.

Katika hatua za haraka za kuhakikisha maji yanawafikia wananchi kwa wakati, Waziri Aweso amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kuhakikisha kuwa kila kijiji kinachopitiwa na bomba la maji kinaanza kupata maji bila kusubiri mradi mzima kukamilika.

Waziri Aweso amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mingine mikubwa ya maji wilayani Mkinga, ikiwemo mradi wa Mkinga - Horohoro wa shilingi bilioni 35.4, mradi wa Gombelo bilioni 3.2, mradi wa Mapatano bilioni 1.5. 

Aidha, ameeleza kuwa mradi huo unatekelezwa na wakandarasi wazawa, akisema Serikali inafarijika kuona wazawa wanapewa nafasi na wanatekeleza miradi mikubwa kwa ufanisi.

Waziri Aweso pia ametangaza kuwa mkandarasi wa mradi huo kwa sasa atakuwa chini ya usimamizi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ili kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Amesisitiza kuwa, Serikali itaendelea kuleta fedha ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati, huku akieleza kuwa kukamilika kwake kutafanikisha upatikanaji wa maji kwa zaidi ya asilimia 90 katika wilaya ya Mkinga.

Kwa uwekezaji huu mkubwa wa Serikali katika sekta ya maji, Mkinga inatarajiwa kuwa miongoni mwa wilaya zenye huduma bora za maji nchini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Rais Samia ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi na salama.