Back to top

CHANZO CHA MAGONJWA ADIMU WATAALAM WATAKIWA KUFANYA TAFITI MPYA

28 February 2025
Share

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, amewataka watafiti na wataalamu wa afya kuangalia upya chanzo halisi cha magonjwa adimu, akisisitiza kuwa kuna haja ya kufanya mchakato mpya wa tafiti ili kupata majibu sahihi kuhusu sababu zinazopelekea magonjwa haya.

Ametoa wito huo leo wakati wa  maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Adimu yaliyofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), akieleza kuwa uelewa wa kina kuhusu vyanzo vya magonjwa haya ni hatua muhimu katika kuboresha matibabu na ustawi wa wagonjwa.

"Wanasayansi wa afya tunatakiwa kufikiria tofauti. Tunahitaji tafiti mpya zitakazotueleza kwa uhakika chanzo halisi cha magonjwa adimu. Bila kuelewa kiini chake, hatuwezi kuwa na tiba sahihi wala mbinu bora za kinga," amesema Prof. Janabi.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, magonjwa adimu huathiri idadi ndogo ya watu ukilinganisha na magonjwa mengine ya kawaida, lakini yana athari kubwa kwa maisha ya wagonjwa na familia zao. Changamoto kubwa ni gharama kubwa za matibabu na upatikanaji mdogo wa dawa.

"Naomba hizi tafiti zetu tutakapozifanya, tuzirahisishe na tunaweza kutoa utangulizi na kuweka kwa lugha ya kiswahili ambayo watu wengi wataifahamu" aliongeza.

Takwimu zinaonyesha kuwa magonjwa adimu mara nyingi husababishwa na hitilafu za vinasaba, mabadiliko ya kimazingira, au maambukizi nadra. Kwa mfano, utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya magonjwa adimu husababishwa na matatizo ya kijenetiki, huku mengine yakiwa na uhusiano na hali za kimazingira kama uchafuzi wa hewa au kemikali hatarishi.