Back to top

TANZANIA, OMAN KUIMARISHA USHIRIKIANO KIDIPLOMASIA

28 February 2025
Share

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Oman ambao umedumu kwa miaka 44 ni wa kihistoria na umeendelea kuwa na manufaa baina ya nchi hizo mbili.

Dkt. Biteko ameyasema hayo ofisini kwake Jijini Dar es salaam wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud Hilal Al Shidhani. 

“ Mhe. Balozi tunakushukuru kwa namna tunavyoshirikiana na uwepo wako nchini umeendelea kuimarisha mahusiano na Serikali yako. Tunafurahia kuwa na uhusiano huu wa kidiplomasia. Sisi tunaichukulia Oman kama marafiki na Mhe. Rais Samia anapenda ushirikiano baina ya Tanzania na nchi zingine;kanuni inayosema ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako ni muhimu sana, amesema Dkt. Biteko.

Ameendelea kusema kuwa uwepo wa idadi kubwa ya Watanzania wanaofanyakazi nchini Oman ni tafsiri  ya urafiki na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo.

Dkt. Biteko amesema kuwa Tanzania itapeleka timu ya wataalamu nchini humo ili kujifunza kuhusu masuala ya gesi pia amemweleza Mhe. Balozi Al Shidhani kuhusu nia ya Serikali ya kufanya mnada wa vitalu vya gesi utakaofanyika katika Mkutano na Petroli wa Afrika Mashariki kuanzia Machi 4 hadi 7 mwaka huu, hivyo mnada huo unaweza kuwa fursa kwa kampuni za kutoka nchini Oman.

Aidha, fursa zingine zinazotokana na ushirikiano huo ni kuendeleza ufadhili wa masomo ya vijana kutoka Tanzania kwa ajili ya kusoma nchini Oman hususan katika masuala ya biashara, mafuta na gesi.

“ Ushirikiano wetu wa Wizara ya Nishati  na Serikali ya Oman haukwepeki katika mnyororo mzima kuanzia uzalishaji hadi katika biashara. Tupo kwenye njia sahihi na tunaamini katika ushirikiano huu tutapiga hatua zaidi na tutaacha alama,” amesema Dkt. Biteko

Akizungumzia kuhusu ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia amesema kuwa nchi za Afrika na nchi zinazoendelea zizungumze lugha moja kuhusu namna ya kuzalisha nishati kwa ajili ya kusaidia watu milioni 600 wanaokosa nishati Barani Afrika kwa kutumia raslimali zilizopo huku akitolea mfano baadhi ya nchi zilizondelea kutumia makaa ya mawe kwa ajili ya kuzalisha umeme lakini kutoruhusu nchi za Afrika kufanya hivyo.

“ Afrika hatufanyi uchafuzi  mkubwa wa hali ya hewa kama kama nchi zilizoendelea na pia kama kuna teknolojia wanayoweza kutupa basi itumike ili kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa, lakini  kiwango cha uchafuzi hakifanani kati ya nchi hizi. Hivyo tunahitaji kuzungumza lugha moja na nimeona baadhi ya nchi za Bara la Asia zinazungumza lugha moja katika hili,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Pia, amezipongeza Kampuni za nchini Oman  zinazofanya biashara Tanzania kwa kuendelea kufanya shughuli zao kwa ufanisi pamoja na kuzikaribisha kuwekeza katika sekta ya gesi kwa kuwa nchi ina kiwango kikubwa cha gesi baada ya kuhamia katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji.

Kwa upande wake, Balozi wa Oman nchini, Mhe. Saud Hilal Al Shidhani amesema kuwa nchi yake inafurahia uhusiano uliopo kati yake na Tanzania na wanajivunia kuwa na watu zaidi ya asilimia 30 wanazungumza Kiswahili kati ya watu milioni 9 waliopo nchini humo.

Balozi Shidhani amesema kuwa nchi yake ina uelewa mkubwa zaidi kuhusu masuala ya mafuta na gesi hivyo inaweza kuisaidia Tanzania kwa kuwajengea uwezo wataalamu wake, halikadhalika Tanzania inaweza kuisaidia nchi yake katika masuala ya madini kwa kuwa imepiga hatua zaidi.

“ Kuna maeneo mengi tunayoweza kushirikiana na Tanzania mfano hapa kuna umeme mna umeme wa ziada na sisi hivi karibuni tumefungua kituo cha kuzalisha hydrojeni na Tanzania inaelekea uelekeo huu hivyo kama kuna fursa mpya tunaweza kushirikiana kwa karibu,” amesema Balozi Shidhani.

Ameongeza kuwa nchi yake imeandaa jukwaa maalum kwa ajili ya kutoa fursa za ufadhili wa masomo kwa Watanzania, pia ameahidi kuchimba visima vya maji 20.