Back to top

URUSI YAONGEZA USHIRIKIANO WA KISAYANSI NA ELIMU NA TANZANIA

10 March 2025
Share

Urusi imesisitiza tena dhamira yake ya kuimarisha uhusiano wa kisayansi, utafiti na elimu na Tanzania katika sekta za mazingira na teknolojia, huku ujumbe wa wajumbe kumi kutoka Urusi ukiwa nchini kama sehemu ya Msafara wa Kisayansi na Kielimu wa Urusi na Tanzania.  

Akizungumza mapema hive Leo, Machi 10, 2025 katika Kituo cha Utamaduni cha Urusi jijini Dar es Salaam, Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Mhe. Andrey Avetisyan, alielezea fursa kubwa zilizopo kwa ushirikiano katika misitu, kilimo, na uhifadhi wa wanyamapori.  

"Tanzania ina zaidi ya hifadhi 22 za taifa, nyingi kati yake hazijajulikana sana kimataifa. Zaidi ya Serengeti na Ngorongoro, kuna mandhari za kipekee ambazo wachache wameziona. Kuna nafasi kubwa ya kushirikiana katika uhifadhi wa mazingira," alisema.  

Ujumbe huo wa Urusi, ukiwahusisha wasomi na watafiti, upo nchini ili kuangaza furs za ushirikiano wa kisayansi, programu za kubadilishana wanafunzi, pamoja na fursa za uwekezaji katika sekta za misitu na kilimo.  

Balozi Avetisyan alibainisha kuwa wahitimu wa vyuo vikuu vya Urusi tayari wanachangia katika juhudi za uhifadhi wa mazingira nchini Tanzania, hususan katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Afrika (Mweka).  

Mratibu wa Ugeni huo, Mhifadhi Jared Otieno kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),, aliukaribisha ujumbe huo wa Urusi na kuelezea furaha yake kuhusu ushirikiano huo uliosubiriwa kwa muda mrefu katika usimamizi wa misitu na uhamishaji wa teknolojia.  

"Tumefarijika sana kuwa wenyeji wenu hapa Tanzania tunapokamilisha ushirikiano huu muhimu. Sekta ya misitu inapanuka, lakini changamoto bado ni nyingi, hasa katika upande wa teknolojia. Uwepo wenu hapa ni hatua kubwa kwetu," alisema Otieno. 
 
Alisisitiza umuhimu wa teknolojia za kisasa kusaidia mashamba ya miti yanayomilikiwa na sekta binafsi pamoja na Serikali na kuhakikisha rasilimali za misitu zinachangia kikamilifu katika uchumi wa taifa.  

Otieno alieleza ratiba ya ujumbe huo, ambao unajumuisha ziara katika miji ya Dodoma, Arusha, na Moshi, ambako watakutana na maafisa wa serikali, taasisi za utafiti, na jamii za wenyeji. Timu hiyo pia itatembelea Hifadhi ya Ngorongoro ili kujifunza jinsi uhifadhi wa wanyamapori, mifugo, na utamaduni wa kiasili wa Wamasai unavyoweza kuunganishwa kwa njia endelevu.  

"Hatulengi tu misitu, bali pia uhifadhi wa mifumo ya ikolojia na jinsi teknolojia inavyoweza kusaidia katika uendelevu wake. Ushirikiano huu lazima uendane na mikakati ya kimataifa ya mazingira ili kuhakikisha mafanikio yake ya muda mrefu," aliongeza.  

Ziara hii inatarajiwa kufungua milango kwa miradi mipya ya utafiti, programu za kubadilishana wanafunzi wa vyuo vikuu, na miradi ya pamoja ya kisayansi, hatua ambayo itaendeleza ushirikiano wa muda mrefu kati ya Urusi na Tanzania.