
Wananchi wa Mkoa wa Mara wamekumbushwa kuwa mikopo inayotolewa na Serikali haitolewi kwa maana ya zawadi bali inatolewa kwa kusudi la kumwinua mwananchi kwa suala la kipato na inatakiwa irudishwe ili wengine waweze kunufaika pia.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala Mkoa wa Mara Gerald Kusaya alipokutana na kufanya mazungumzo na Timu ya Wataalamu ya Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha.
Kusaya amewataka wananchi wa mkoa huo kutumia mikopo inayotolewa na Serikali kwa manufaa na kuirejesha kwa wakati ili iweze kuwanufaisha wengine wenye uhitaji.
Bw.Kusaya alisema kuwa Serikali imekuwa na mpango mahususi wa kutoa mikopo kwenye vikundi kupitia Halmashauri, lakini utafiti unaonesha kuwa pamoja na jitihada za Serikali kuna watu hawajanufaika na mikopo hiyo kutokana na uelewa mdogo wa masuala ya mikopo.
Kwa upande mwingine w. Kusaya alishangazwa na tabia za wananchi kukopa kwenye taasisi za “mikononi” ambazo hazina ofisi, ambazo ni dhahiri kuwa ufuatiliaji wa marejesho hauwezi kuwa na ustarabu, alisema taasisi ya ukopeshaji ni lazima iwe na ofisi, anuani na usajili.
Awali Kiongozi wa Timu ya wataalamu wa utoaji wa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw. Salim Kimaro, alisema Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini, wametakiwa kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2025/2026 asilimia 85 ya wananchi iwe imefikiwa na elimu hiyo.