Back to top

SERIKALI YATOA MWONGOZO MLIPUKO WA MPOX

11 March 2025
Share

Wizara ya Afya nchini Tanzania imetoa muongozo kwa wasafiri kufuatia mlipuko wa Homa ya Nyani (MPOX), ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia Kanuni za Afya za Kimataifa za mwaka 2005, ambapo muongozo huo unaanza kutekelezwa mara moja, ili kuchukua hatua madhubuti zinazohusiana na wasafiri wa Kitaifa na Kimataifa.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif A. Shekalaghe kwa vyombo vya habari, imebainisha kuwa Wasafiri na wafanyakazi wote katika maeneo ya mipakani wanapaswa kuzingatia hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi kama vile unawaji wa mikono, kuacha angalau umbali wa mita moja baina ya mtu mmoja na mwingine, na kutoa taarifa kuhusu mtu yeyote mwenye dalili za ugonjwa kwa kupiga simu namba 199 bure, kutoa taarifa ofisi ya afya mipakani au kituo cha afya kilicho karibu.
 
Pia Katika maeneo yote ya mipaka (viwanja vya ndege, mipaka ya nchi kavu na bandari), wasafiri wote watafanyiwa uchunguzi wa awali wa afya ikiwamo kupimwa joto la mwili na watakaobainika kuwa na homa na au vipele watafanyiwa uchunguzi wa kina wa kiafya.

Kadhalika Elimu kuhusu utoaji wa taarifa mapema na ushauri wa afya kuhusu kuripoti dalili zozote za ugonjwa wa Mpox itatolewa kwa wasafiri wote mipakani. Wale watakaoonesha dalili hizo watafanyiwa uchunguzi wa kina na kupatiwa matibabu katika vituo vya huduma za afya.

Hata hivyo, watu wote waliotangamana na wagonjwa wa Mpox watashauriwa kufuatilia afya zao na kutoa taarifa katika kituo cha afya kilicho karibu au kupiga simu namba 199 bure iwapo watakuwa na dalili zozote za Mpox.

Aidha Wasimamizi na Wamiliki wote wa vyombo vya usafiri pamoja na madereva wanapaswa kufuata taratibu za kiafya zikiwamo uchunguzi wa afya, ukaguzi wa usafi wa vyombo vya usafiri, kunawa mikono, matumizi ya vitakasa mikono, na kutoa taarifa mara moja kuhusu msafiri yeyote mwenye dalili za Mpox kwa mamlaka za afya mipakani.