
Wakuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mikoa na Vikosi kutoka Tanzania bara na Zanzibar, wametakiwa kutilia mkazo upelelezi wa makosa ya uhalifu wa kifedha kwa kutumia mbinu mpya ili kuifanya Tanzania kuendelea kuwa salama dhidi ya makosa hayo.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini DCI Ramadhan Kingai, ameeleza hayo leo wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya Upelelezi wa makosa ya kifedha kwa Wakuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mikoa (RCO's) na Vikosi (DCO's) yanayofanyika Jijini Dodoma.
DCI Kingai amesema RCO's na DCO's ni watu muhimu katika kuhakikisha kuwa makosa ya kifedha yanadhibitiwa na hilo litafanikiwa kutokana na upelelezi makini na mbinu za kisasa jambo ambalo litafanya kesi za makosa hayo kupata mafanikio mahakamani.
Kwa upande wake Naibu DCI, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Saleh Ambika, amesema mafunzo hayo ni muhimu hususani katika kipindi hiki ambacho Jeshi la Polisi linaendelea kufanya maboresho ikiwemo matumizi ya TEHAMA katika upelelezi.
Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Makosa dhidi ya fedha (FCU) Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Hapiness Laizer, amesema mafunzo hayo yataboresha utendaji kwa kuwa wakufunzi wanatoka katika Taasisi mbalimbali zinazohusika na makosa hayo ya kifedha.
SSP Laizer amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa kwa wapelelezi na yanaendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha kuwa makosa hayo yanadhibitiwa hapa nchini.