
Wizara ya Afya imewasilisha vipaumbele 11 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ambavyo ni pamoja na kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko na magonjwa yasiyoambukiza, kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa kwenye ngazi za msingi hadi Taifa.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amewasilisha vipaumbele hivyo, mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ikiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mheshimiwa Dkt. Christine Mnzava.
"Vipaumbele hivi ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea na utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, kuimarisha tafiti na matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za afya, huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto," amesema Waziri Mhagama.
Vipaumbele vingine amevitaja kuwa ni kuimarisha upatikanaji na uendelezaji wa wataalam wa Sekta ya Afya kwa fani za kati, ubingwa na ubingwa bobezi, kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi, pamoja na kuimarisha Tiba Utalii nchini.
Vipaumbele vingine ni kuendeleza na kusimamia afua za tiba asili na tiba mbadala, kuimarisha upatikanaji wa huduma za tiba dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa ya mlipuko.