Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu imeyatupilia mbali maombi ya mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na wenzake nane ya kutaka kesi yao iende Mahakama Kuu kwaajili ya kupata tafsiri ya kisheria kuhusu uhalali ya kushitakiwa kwa makosa ya jinai wakati wakitekeleza majukumu yao kikatiba kwa sababu hayana mashiko.
Uamuzi huo umetolewa na hakimu Mkazi Mkuu, Wilbad Mashauri na kuipanga kesi hiyo ianze kusikilizwa kuanzia Mei 16,2018 saa nane mchana kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali.
Mahakama imetoa uamuzi huo mbele ya washtakiwa, Freeman Mbowe, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba John Mnyika,
Mbunge wa Tarime mjini Esterher Matiko, kKtibu wa Chama hicho Dkt.Vicenti Mashinji na mbunge wa Tarime vijijini, John Heche.
Katika kesi hiyo washtakiwa Eshter Bulaya na mbunge wa Kawe Halima Mdee hawakuwepo Mahakamani ambapo kwa mujibu wa wakili wa upande wa utetezi Peter Kibatala ameiambia mahakama kuwa walipatwa na tatizo katika gari wakati wakiwa njiani wakitokea Dodoma kuja Dar es Salaam.
Aidha ameiomba mahakama kuipanga kesi hiyo kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali Juni 8 ama 15, 2018 ombi ambalo lilipingwa na upande wa mashtaka na kuiomba mahakama washtakiwa hao wasomewe wasomee maelezo ya awali mei 16,2018 mwaka huu.
Kutokana na hoja za upande wa utetezi na mashtaka kuhusu tarehe ya kusomwa kwa maelezo ya awali, hakimu Mkazi Mkuu Wilbad Mashauri ameiahirisha kesi hadi mei 16,2018 saa nane mchana ambapo washtakiwa hao watasomewa maelezo ya awali.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 12 katika kesi ya jinai namba 112 ya mwaka 2018 ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria na kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali ama maandamano yaliyosababisha kifo cha Akwilina.
.